Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Ndugu Brown Mwangomale amefanya ziara ya kuimarisha uhai wa chama hicho wilayani Mufindi kwa lengo la kukagua ujenzi nyumba ya katibu wa CCM wilaya ya Mufindi. Katika ziara hiyo, Mwangomale ambaye aliongozana na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Sadick Kadulo ameagiza ujenzi wa nyumba hiyo uanze mara moja baada ya kusimama kwa miaka mingi, bila kuendelezwa. Pia, Mwangomale ametembelea viwanja viwili vya CCM vilivyopo karibu na kituo cha Polisi na kuishauri CCM Wilaya ya Mufindi kujenga hoteli ya kisasa, itakayosaidia kuongeza mapato. Akizungumza baada ya ziara hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi, James Mgego ameahidi kutekeleza maagizo ya Mwangomale na kwamba ameahidi kusimamia ujenzi wa nyumba hiyo sambamba na uendelezaji wa viwanja vya CCM. Kuhusu uwanja wa Mpira, Mwangomale ameiomba CCM Makao Makuu kusaidia ujenzi wa kisasa kwenye uwanja huo ili kuendeleza sekta ya michezo ndani ya mkoa wa Iringa.